Home » » Waraka wa Pili wa Mbunge kwa Wananchi wa Jimbo la Ubungo

Waraka wa Pili wa Mbunge kwa Wananchi wa Jimbo la Ubungo


Uhuru na Kazi:Nimekuja kuwatembelea kuona hali halisi ya uharibifu wa makazi yenu, mali zenu na miundombinu yetu kutokana na maafa ya maafuriko katika mitaa hii ya kata ya mabibo. Kuanzia maafa yatokee tarehe 20 Disemba mpaka tarehe 24 Disemba nimekuwa pamoja na wananchi wenzangu wa jimbo la Ubungo bega kwa bega katika jitihada za uokoaji na utoaji wa huduma za kijamii katika maeneo mbalimbali mathalani Msewe, Ubungo, Kisiwani, Kibo, Mburahati, Sinza D, Sinza E, Uzuri, Manzese Chakula Bora, Mburahati Kisiwani, Msigani, Mbezi Kibanda cha Mkaa, Kimara B. Na pia, nimeenda kutoa misaada kwa majimbo jirani ya Kinondoni (Magomeni Sunna na Kigogo), Kawe (Msasani Bonde la Mpunga na Bunju) na Ilala (Mchikichini). Kutokufika Mabibo, katika hizo siku chache, kunadhihirisha ukubwa wa maafa yenyewe na ilikuwa vigumu kuwepo mahali pote wakati wote. Hata hivyo, katika wakati huo wote nilikuwa na mawasiliano na wananchi na viongozi kuhakikisha kwamba mamlaka zinazohusika na uokoaji zinafika katika maeneo haya. Nawashukuru wote mliotoa ushirikiano wakati wa uokoaji na nawashukuru pia mliotoa msaada wa hali na mali kwa majirani zenu katika kipindi hiki kigumu.

Nimekuja kwenu leo katika sikukuu ya kufungua zawadi (boxing day) kutoa michango yangu ya chakula na mavazi kwa waathirika wa maafa wasio na uwezo; hata hivyo zawadi yangu kubwa kwenu leo; sio vitu hivi tulivyotoa, ni waraka ninaoutoa kwenu wananchi wenzangu wa jimbo la Ubungo. Waraka huu naamini utakuwa ‘chakula’ cha fikra kwenu leo na kesho kwa ajili ya mabadiliko katika maisha yetu na taifa letu.

Katika waraka wangu wa kwanza kwenu niliwapa mrejesho kuhusu uwakilishi wa Mbunge katika mkutano wa pili wa Bunge. Nawaandikia waraka huu “Uhuru na Mabadiliko” katika mwaka 2011 wa kumbukumbu ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika ambayo sasa inaitwa Tanzania bara.

Lengo la waraka huu ni kuungana nanyi katika mwaka huu kutafakari kila mmoja wetu kuhusu taifa letu lilipotoka, lilipo na tunapotaka liende katika kipindi cha miaka 50 toka Uhuru na kutumia fursa hiyo pia kutafakari kuhusu jimbo letu katika kipindi cha mwaka mmoja toka uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na kuwatakia heri ya mwaka mpya wa 2012.

Waraka huu wote, isipokuwa aya ya kwanza na aya hii ya tatu, niliuandika tarehe 9 Disemba 2011; hata hivyo sikuutoa siku hiyo kutokana na ‘macho na masikio’ ya wengi kuelekezwa katika ‘sherehe’ za siku hiyo pamoja na matarajio kuhusu hotuba ya Mkuu wa Nchi kugusa masuala mapana kuhusu mwelekeo wa taifa. Nimeona niutoe waraka huu katika kipindi cha kuelekea mwisho wa mwaka, na ni wakati muafaka wa kutafakari zaidi baada ya ‘sherehe’ kwa kuwa mpaka sasa Rais Jakaya Kikwete hajatoa hotuba nyingine ndefu kama alivyoahidi tarehe 9 Disemba na pia taifa linamaliza majonzi yaliyotokana na maafuriko yaliyoleta maafa katika mkoa wa Dar es salaam.

Kwa hali hii ni wakati muafaka wa kurudi nyuma na kutafakari kiwango cha fedha tulichotumia kwenye ‘sherehe’ za uhuru; huku taifa likiwa halina hata vifaa vya msingi vya uokoaji wakati wa maafa. Ni wakati muafaka wa kutafakari, ‘mafanikio’ ya miaka 50 ya uhuru, tukiwa na matatizo ya mipango miji na kutetereka kwa misingi ya utawala wa sheria katika mkoa wa Dar es Salaam ambao ulitangazwa kuwa jiji mwaka huo huo wa uhuru.

Nashukuru kwamba waraka huu nautoa kwa mara ya kwanza hadharani kwenye kata ya Mabibo jirani kabisa na eneo la Loyola ambalo linabeba kumbukumbu ya kihistoria kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kwa Jimbo la Ubungo. Hivyo Nitatumia vile vile waraka huu na fursa hii kuwadokeza baadhi ya wajibu wa msingi ambao mbunge ameutekeleza katika Jimbo la Ubungo katika kipindi cha mwaka mmoja.

Naelewa kwamba wapo wengine ambao walitumia mwaka huu wa 2011 wa maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru kufanya ‘sherehe’ ama kufanya ‘maonyesho ya kijeshi’, lakini binafsi nimeona pamoja na yote niwaandikie tutumie kutafakari. Ni wakati wa kila mmoja wetu kujiuliza ameifanyia nini nchi na pia kujiuliza nchi na wananchi wenzake wamemfanyia nini katika miaka 50 ya uhuru wetu. Tafakari hii haiwezi kuwa ya siku moja ya tarehe 9 Disemba bali ni mchakato endelevu wa kujimbua na kuchukua hatua. Tuna kila sababu ya kukumbuka na kuadhimisha siku ya uhuru, lakini hatuna sababu nyingi za kusherehekea tena kwa gharama kubwa tukilinganisha baina ya umri, rasilimali na mafanikio tuliyoyapata.

Tunaelezwa kwamba Tanganyika ilipata uhuru bila kupigana vita hivyo maonyesho ya kijeshi ni ishara tu ya kujipanga kwetu katika kulinda uhuru wa mipaka yetu; lakini ilipaswa sikukuu ya leo iwe ni ya kuonyesha matunda ya miaka 50 ya uhuru.
Mwaka 1958 wakati Mwalimu Julius Nyerere akihutubia Umoja wa Mataifa (UN) kutaka Uhuru wa Tanganyika dhidi ya mkoloni alieleza kwamba tunapodai uhuru kutoka kwa Waingereza sio kwamba tunataka ili watupe tu utawala, bali ni kwa sababu wameshindwa kuondoa umaskini, wameshindwa kuelimisha Watanganyika na pia wameshindwa kutoa huduma za afya.

Tarehe 9 Disemba 1961 kupitia hotuba zake mbili kwa nyakati na matukio tofauti Nyerere akarudia kuwatangaza maadui watatu wa taifa- umaskini, ujinga na maradhi na akataka kila mmoja awapige vita. Siku hiyo hiyo, Nyerere akatangaza kuwa adui mkubwa ni umaskini! Miaka michache baada ya uhuru akarejea kumtaja adui mwingine mkubwa zaidi ambaye aliwahi kumweleza hata wakati wa kudai uhuru; naye ni ufisadi. Kwa hiyo vita yetu kwa sasa ni ya maadui wanne; ufisadi, umaskini, ujinga na maradhi. Katika kutathmini tulipotoka, tulipo na kupanga tunapotaka kwenda ni muhimu tukawatazama maadui hawa miongoni mwetu wananchi na katika nchi yetu kwa ujumla.

Nawashukuru tena kwa kunipa heshima ya kunituma kuwawakilisha na kuwatumikia kwa kadiri nilivyowaomba kupitia uchaguzi ili kuunganisha nguvu za pamoja katika masuala ya kitaifa bungeni lakini pia tukiweka mkazo katika utekelezaji wa ahadi jimboni kwa kuweka kipaumbele kwenye; Akili, Ajira, Miundombinu, Maji, Uwajibikaji, Usalama, Ardhi na Afya (AMUA).

Kimsingi kazi tatu kuu za mbunge ambazo zinatokana na mamlaka ya bunge kwa mujibu wa ibara ya 63 ya katiba ni; Mosi kuwakilisha (representation) wananchi, pili ni kutunga sheria (legislative) na tatu ni kuisimamia serikali (oversight) kuweka mazingira bora ya maendeleo kwa mwananchi mmoja mmoja na nchi kwa ujumla.
Kama sehemu ya uwakilishi na usimamizi mbunge ana wajibu pia wa kuunganisha nguvu ya umma jimboni kuhamasisha maendeleo kupitia mfuko wa maendeleo ya jimbo na wadau wengine.

Mwishoni mwa mwaka tutatoa Jimboni Ubungo taarifa ya kina ya utekelezaji ya kata kwa kata lakini katika waraka huu nitaeleza baadhi katika muktadha wa kutafakari mabadiliko ya nchi yetu kiuchumi, kisiasa na kijamii miaka 50 baada ya Uhuru wa Tanganyika.

Wakati wa uhuru taifa hili lilikuwa na watu chini ya milioni 10; sasa Dar es salaam pekee ina wananchi takribani milioni nne, karibu nusu ya Tanzania ya wakati huo ikiwa Tanganyika. Miaka 50 ya Uhuru sasa taifa lina watu wanaokaribia milioni 50; hivyo taifa letu watu wake zaidi ya robo tatu ni kizazi cha baada ya uhuru. Maanake katika kila watu kumi tunaopishana nao barabarani, zaidi ya saba ni kizazi cha baada ya uhuru.

Pamoja na kuwa harakati za uhuru zilifanyika kona zote za nchi wakazi wa Jiji la Dar es salaam lenye umri wa miaka 50 tunabeba historia ya pekee ya harakati hizo ziliratibiwa kwa busara za wazee wenye imani kuwa vijana ni nguvu ya mabadiliko. Baadhi ya vijana hao kama Chifu Patrick Kunambi waliweka makazi yao katika Jimbo la Ubungo wakati huo kwa sehemu kubwa likiwa mapori.

Ni wazee wa Dar es salaam ndio waliomuita Mwalimu Nyerere toka Pugu, kwa mchango wao wa hali na mali, kijana wao, akawa mwenyekiti wa taifa wa chama cha wakati huo cha TANU akiwa na miaka 32, akaongoza harakati za uhuru, mpaka nchi ikapata uhuru. Akaongoza nchi hii vizuri katika miaka ya kwanza ya uhuru, akiweka misingi ya muda mrefu ya taifa yenye kutazama mbele kwa miaka mingi kiuchumi, kisiasa na kijamii; misingi ambayo wenzake wameitupilia mbali.

Waraka huu ni kwa ajili ya wote wenye kuamini kwamba uhuru wa kweli, si uhuru wa bendera bali ni uhuru dhidi ya umasikini, ujinga, maradhi na ufisadi. Uhuru wa kweli, ni uhuru wenye kuleta maendeleo kisiasa, kijamii na kiuchumi. Uhuru huu ni wenye mabadiliko ya kweli, yenye kuhimili misukosuko ya ukoloni mamboleo; na kujenga taifa lenye kutumia vizuri rasilimali katika kutoa fursa kwa raia wake. Uhuru na Kazi, Uhuru na Mabadiliko.

Uhuru na Mabadiliko ya Uchumi:
Katika kufakari tulipotoka, tulipo na tunapotaka uchumi wetu ufike miaka 50 baada ya uhuru tunapaswa kukumbuka kwamba dhamira ya kudai uhuru ilikuwa ni nchi kujitegemea kiuchumi na kuweka mazingira ya mabadiliko katika maisha ya wananchi kiuchumi. Katika hotuba zake mbili za tarehe 9 Disemba 1961, Nyerere alisisiza kwamba tukiweza kupambana na umaskini tutaweza kupata silaha ya kupambana na ujinga na maradhi.
Katika kutimiza azma hiyo taifa lilihamasishwa kufanya kazi , kujitegemea na pia kutumia vizuri rasilimali za taifa. Katika kufanya hivi Nyerere alitambua ‘utajiri wa Tanganyika bado uko ardhini’ na kusisitiza ‘ni juu yetu tuijenge Tanganyika sisi wenyewe zaidi kwa kutumia utajiri tulionao na kwa juhudi zetu wenyewe’ . Miaka 50 ya uhuru tumeruhusu utajiri huo utoke ardhini lakini hatujaweza kuutumia vizuri kukuza uchumi wa nchi na kubadili maisha ya wananchi.

Tukitumia kipimo cha umaskini cha wastani wa pato kwa mwananchi, miaka michache baada ya uhuru wastani wa pato lilikuwa dola nne; lakini miaka 50 baada ya uhuru sehemu kubwa ya watanzania wanaishi chini ya dola moja kwa siku hali ambayo inaonyesha kuwa umaskini umeongezeka huku gharama za maisha zikizidi kupanda. Nyerere aliwahi kuhimiza kwamba maendeleo ya kweli ni ya watu sio ya vitu; hivyo miaka 50 baada ya uhuru vitu vinaweza kuwa vimeongezeka lakini ukilinganisha maisha ya watu taifa lina changamoto kubwa ya kushughulikia.

Katika kutekeleza wajibu wa uwakilishi na usimamizi nimefuatilia bungeni na jimboni kwa njia mbalimbali kuhusu kupanda kwa gharama za maisha kunakochangiwa na mfumuko wa bei pamoja kuporomoka kwa thamani ya shilingi. Jambo ambalo limenisukuma kutoa mwito kwa serikali kuandaa mpango wa dharura wa kunusuru uchumi na kupunguza gharama za maisha kwa wananchi. Hatimaye serikali imetoa kauli ya kuandaa mpango wa haraka wa kushughulikia suala hili. Nitaendelea kufuatilia kwa karibu ili mpango huu uwasilishwe bungeni na utekelezaji uanze.

Ikumbukwe kwamba katika mkutano wa bunge la bajeti nilipinga ongezeko la kodi kwenye mafuta ya taa na kuwasilisha jedwali la marekebisho kwenye muswada wa Sheria ya Fedha ili kupunguza kodi ya petroli na dizeli kwa ajili ya kupunguza bei kwa mteja. Hata hivyo, uwingi wa wabunge wa CCM ulitumika kupinga mapendekezo haya ambayo nitaendelea na hatua ya kuyasukuma kufuatia pia maamuzi ya vikao vya juu vya chama hicho kuendana na misingi ya marekebisho niliyoyapendekeza awali.

Kwa upande mwingine, nitaendelea na hatua niliyoianza ya kuwakilisha bungeni muswada binafsi wa sheria kwa ajili ya kudhibiti bei ya bidhaa muhimu. Aidha, nitaendelea kushirikiana na wadau wengine wenye kutaka nchi iongeze uzalishaji kwa kupitia mpango maalumu kwa wazalishaji wadogo katika kilimo na viwanda ili kuchangia katika mauzo ya nje ya kuboresha urari wa biashara na wakati huo huo kupanua wigo wa ajira hususani kwa vijana. Kadhalika, nitaendelea kuunganisha nguvu na wote wanaotaka serikali ibane matumizi na kushughulikia ubadhirifu ili kuokoa uchumi na kupunguza athari za gharama za maisha kwa wananchi. Kupinga posho za vikao na kukataa aina zote za ufisadi ni sehemu ya kuchangia katika jitihada hizo kwa maendeleo ya wananchi wa Ubungo na taifa kwa ujumla.

Miaka ya mwanzo ya Uhuru nchi ilikuwa katika mkondo sahihi wa kiuchumi wa kuweka msukumo katika uzalishaji na manunuzi ya ndani. Kasoro pekee ya Nyerere lilikuwa ni kuweka mkazo sana kwa dola kwa maana ya serikali kumiliki njia za uzalishaji; badala ya uchumi kimilikiwa na umma. Kosa hili lilifanya serikali ishindwe kubeba mzigo mkubwa wa kusimamia sera kisiasa wakati huo huo kufanya utekelezaji kwa kuendesha njia za uzalishaji mali za kiuchumi wakati huo huo ikiwa inatoa huduma za kijamii.
Kwa ujumla pamoja na kuimba haja ya kujitegemea, dola ikazalisha raia wategemezi kifikra, ambao chini ya mfumo wa chama kimoja na mwelekeo dhaifu wa kiuchumi; walipoteza ujasiri wote wa ushindani. Ni hali hii ndio ilifanya wengine kuanzisha vyama mbadala yenye kuamini katika mfumo wa soko la kijamii; lenye kuhakikisha kwamba uchumi unamilikiwa na wananchi.

Huu ni mfumo wa kiuongozi wa kisera na kirasilimali ambao unahakikisha kuwa rasilimali za nchi zinatumika kwa manufaa ya maisha ya wananchi wake; kwa kujenga taifa lenye kutoa fursa.

Lakini afadhali kosa la Nyerere linaweza kusameheka miaka 50 baada ya uhuru, lakini makosa ya warithi wake, baada ya kung’atuka kwake na baadaye kufa kwake yameacha majeraha makubwa yanayohitaji taifa hili likombolewe upya miaka mingi ijayo.

Awamu zilizofuata za utawala zikaruhusu kusukumwa fikra za kifisadi na utupu wa kiitikadi, kuindoa nchi katika ujamaa wa dola na kuitumbukiza katika soko holela badala ya soko la kijamii.

Chini ya sera dhaifu na ubinafsi wa viongozi wake, njia za uzalishaji mali zikauzwa kwa bei chee; toka kwa dola kwenda kwa wageni, na kwa tabaka la wachache linalojifunika kwa kivuli cha mabepari uchwara wa ndani; wengi wao wakiwa kwenye korido za chama tawala na serikali yake.

Wakati wa Uhuru tarehe 9 Disemba 1961 pamoja na kuwa nchi ilikuwa na vyama vingi vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi katika hotuba zake zote mbili Mwalimu Nyerere alitambua umuhimu wa chama kilicho madarakani katika kuongoza nchi, na kueleza wajibu wa TANU baada ya uhuru. Ukitathmini miaka 50 baada ya uhuru utabaini kwamba miaka 50 baada ya Uhuru chama kilikabidhiwa wajibu huo cha CCM kimeutelekeza badala ya kuutekeleza jambo ambalo linapaswa kuunganisha watanzania wote bila kujali vyama kufanya mabadiliko ya kimfumo.

Mathalani miaka 50 baada ya uhuru, watanzania wanaendelea kupotoshwa kwamba Taifa letu linafuata siasa ya ujamaa na kujitegemea suala ambalo linatajwa pia katika katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni wazi chama kilichopo madarakani kinapotawala huku kikiwa na ombwe na kiitikadi na kufilisika kimaadili ni lazima taifa litakuwa na uongozi dhaifu na kuathirika kiuchumi.

Na kwa kweli si maneno yangu, ni ukweli uliosemwa na Muasisi wa TANU na CCM, mwandishi wa Azimio la Arusha, Hayati baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ambaye aliandika katika kitabu cha Uongozi Wetu na Hatma ya Tanzania, namnukuu: “Halmashauri Kuu ya Taifa iliketi Unguja ikabadili Azimio la Arusha bila kwanza kutafuta maoni ya wananchi. Na walikuwa na haki ya kufanya hivyo, maana sera ni yao, ubaya wao ni kwamba jambo lenyewe walilifanya kwa hila na janja janja, na hadi sasa wanaendelea kuwadanganya wananchi kwamba sera ya CCM bado ni Ujamaa na Kujitegemea”

Udhaifu huo wa kifikra ukachanganyika na uozo wa kimaadili na kufanya miaka 50 baada ya uhuru tushuhudie viwanda vikiuzwa kwa bei ya kutupa na vingine kugeuzwa magofu baada ya kuuzwa kwake hali ambayo imechangia katika kuingia kwenye ukoloni mamboleo wa kiuchumi; wa kutegemea kuwa bidhaa za nje na kutegemea kusafirisha bidhaa ghafi kwenda nje ya nchi.

Jimboni Ubungo viwanda mbalimbali ambavyo vilianzishwa na Nyerere mara baada ya uhuru mathalani kiwanda cha Zana za Kilimo (UFI), Kiwanda ca Ubungo Maziwa, Kiwanda cha Nguo Urafiki na viwanda vingine vimeuzwa kinyemela na kubadilishwa matumizi ama kuanza kufilisiwa hali ambayo imeathiri uchumi wa nchi hususani kupunguza mapato ya serikali, kuongeza bidhaa za kutoka nje katika soko letu la ndani na pia kupunguza fursa za ajira.

Mara baada ya kuchaguliwa nimetembelea katika kiwanda cha Nguo cha Urafiki na kufanya mazungumzo na wafanyakazi na kubaini kwamba kiwanda kinazidi kudidimia; nyumba za wafanyakazi ziliuzwa kinyemela kwa kivuli cha ubinafsishaji, mpaka mitambo mingine imeuzwa kama chuma chakavu; pamoja na wafanyakazi kulipwa mishahara duni hata maghorofa ya wafanyakazi yanaendeshwa kibiashara badala ya kuwa huduma ya msingi kwa wafanyakazi.

Kufuatia hali hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja nimefanya kazi ya uwakilishi na usimamizi ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa njia mbalimbali za kibunge na mawasiliano na serikali. Suala la malipo pungufu ya wafanyakazi kufuatia likizo ya lazima kutokana na ukosefu wa pamba nililifuatilia na hatimaye wakapata nyongeza. Kufuatia hatua hizo, kamati ya bunge ya viwanda na biashara nayo imetembelea kiwanda na kuthibitisha masuala ambayo tumeyasema bungeni wakati wa bunge la bajeti na kamati hiyo imetangaza kuunda kamati ndogo kwa ajili ya kufanya uchunguzi zaidi na kuisimamia serikali kuchukua hatua zaidi. Aidha, nitaendelea kuifuatilia serikali kuchukua hatua husususani kupitia Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) pamoja na Wizara zote husika kuhusu viwanda vilivyopo Jimboni Ubungo vilivyobinafishwa kiholela ili kushughulikia matatizo ya muda mrefu ya wafanyakazi, kupanua wigo wa ajira hususani kwa vijana na kuongeza uzalishaji wa bidhaa na mapato kwa serikali.
Miaka 50 baada ya uhuru viwanda vyetu vinaendelea kufa huku tukilazimishwa kisera kujibidiisha kuwa watafutaji wa malighafi na kuzisafirisha kwenda viwanda vya nje zikiwa ghafi na hivyo kushindwa kuwa na uwiano wa kimalipo (Balance of Payment). Wakati tukiua viwanda vya ndani na kupunguza uzalishaji; tunafungua mipaka yetu kwa kiwango cha ajabu na kuingiza bidhaa za nje zikiwemo zisizokuwa na kiwango. Taratibu tunajenga uchumi wa kuwa wachuuzi wa bidhaa kutoka nje. Huo sio uhuru wa kiuchumi ambao waasisi wa taifa hili waliupigania.

Tumehadithiwa na wazee wetu, kwamba wakoloni walitutawala ili kupata nguvu kazi ya bei chee; kupata malighafi kwa ajili ya viwanda vyao na kupata masoko kwa ajili ya bidhaa zao. Tulipotafuta uhuru, ilikuwa ni dhamira yetu kuondoa udhalili huu. Hali imeanza kurejea kwa ari, nguvu na kasi zaidi na kutia doa katika sherehe za miaka 50 ya Uhuru.

Ukoloni mamboleo ndani ya taifa lenye uhuru wa bendera; ndio unaofanya wafanyakazi kutoa nguvu kazi yao kwa bei chee kwa kulipwa mishahara midogo na kupata maslahi duni hususani katika makampuni makubwa ya kigeni ukilinganisha na wafanyakazi toka nje. Sasa utumwa huo unabisha hodi kwa wakulima, kupitia mikakati mipya ya kilimo inayoendelezwa hivi sasa yenye kupokonya ardhi (land grabbing) kwa watanzania wa kawaida kwa kisingizio cha kupanua mashamba kumbe mwishowe watanzania watakuja kuwa manamba. Kumiliki ardhi ni ishara kuu ya uhuru wa wananchi, hivyo tunapokwenda tunapaswa kurekebisha hali hii kwa haraka.

Kwa upande wa Jimboni Ubungo katika kipindi cha mwaka mmoja nimefanya kazi ya uwakilishi katika masuala yanayohusu migogoro na usimamizi wa ardhi kwa ujumla. Nimekuwa sambamba na wananchi wanaodai fidia ya ardhi zao ama wenye migogoro mbalimbali ya ardhi kwa kuwasilisha masuala yao kwenye mamlaka husika na wengine kuwawezesha kupata ushauri wa kisheria. Pamoja jitihada hizo bado migogoro ya ardhi katika kata za pembezoni ni mingi suala ambalo linahitaji kutazamwa kwa ukaribu zaidi. Nimeongeza nguvu zaidi katika kutaka viwanja vya umma vilivyovamiwa viweze kurejeshwa kupitia bungeni na kwenye manispaa kwa kutaka ripoti ya uchunguzi juu ya maeneo hayo iwekwe hadharani na hatua zichukuliwe.

Kutokana na jitihada hizo tayari baadhi ya masuala yaliyofanywa siri awali ya ripoti hizo yamejadiliwa na baraza la madiwani na pia baadhi ya viwanja hivyo tayari vimewekewa mabango ya ilani kuonyesha kwamba ni maeneo yaliyovamiwa. Sasa hatua madhubuti zinazopaswa kuchukuliwa ni kuhakikisha viwanja hivyo vinarejeshwa na hatua stahiki zinachukuliwa kwa wahusika ili kuweka misingi ya uwajibikaji ya kulinda rasilimali za umma.

Matumizi bora ya ardhi yanahitaji kuweka mkazo katika mipango miji pamoja na kuongeza kasi ya upimaji wa maeneo na utoaji wa hati za viwanja hali ambayo itawezesha pia kutoa fursa kwa wananchi kuweza kuzitumia nyaraka hizo kwa ajili ya kujiendeleza kiuchumi na kuongeza thamani ya mali zao. Kwa hali ilivyo sasa jiji la Dar es salaam lina maeneo mengi hatarishi katika mabonde, kingo za mito, karibu na mitambo na viwanda na kwa ujumla katika sehemu zisizopimwa. Hali hii inafanya jiji lisiwe salama panapotokea hatari ya moto, maafuriko na majanga ya aina nyingine. Tumefika hapa tulipo kutokana na udhaifu katika mipango miji na kutokusimamiwa kwa utawala wa sheria. Katika mwaka 2012 na kuendelea lazima tusukume utamaduni wa uwajibikaji. Ni muhimu maeneo yote hatarishi yakatambuliwa na serikali ikaweka utaratibu wa kuyakinga maeneo husika dhidi ya majanga na kwa maeneo ambayo ni vigumu kuyakinga kwa ujenzi wa miundombinu serikali ihakikishe wananchi husika wanakwenda kwenye makazi mbadala. Hatua hii ni muhimu sana katika wakati huu ambao jiji la Dar es salaam kama ilivyo nchi kwa ujumla inapaswa kubadilika kimipango katika kukabiliana pia na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Kutokana na kupungua kwa ajira katika viwanda na aina nyingine za uzalishaji, wapo wananchi ambao wamejiajiri katika kufanya biashara katika ngazi mbalimbali. Hata hivyo, kundi la wafanyabiashara ndogo ndogo hawana uhuru wa kufanya biashara kutokana na kukosa maeneo mazuri ya kufanyia biashara zao.

Katika kipindi cha mwaka mmoja nimefanya kazi ya kuwawakilisha watengewe maeneo maalum ya biashara na kuwatetea wasihamishwe kwenye maeneo wanayofanyia biashara hivi sasa mpaka watakapotengewa maeneo muafaka ya kufanyia biashara zao. Tumefanikiwa kwa manispaa kutenga baadhi ya maeneo lakini kwa kuwa hayajitoshelezi nimewasilisha pendekezo kwa serikali bungeni kutenga kutoka maeneo ya viwanda yaliyotekelezwa ili tupate eneo la viwanda vidogo pamoja na biashara kupanua wigo wa ajira kwa wanawake na vijana.

Suala la kuweka mkazo kwa wazalishaji wadogo nililipa mkazo pia wakati nikitimiza wajibu wa kibunge wa kutunga sheria kupitia marekebisho ya Sheria ya Maeneo Maalum ya kiuchumi na biashara sanjari na kutaka viwanda vinavyowekeza katika maeneo hayo kuanza kulipa kodi mapema zaidi na kupanua wigo wa ajira.

Ukiondoa ongezeko la ujenzi wa barabara kuu miaka 50 baada ya Uhuru; miundombinu mingine imeachwa hohehahe. Hali ya usafiri wa reli inazidi kuwa mbaya usafirishaji wa abiria na mizigo kwa njia hii unazidi kupungua mwaka hadi mwaka. Serikali inazidi kuingiza fedha za walipa kodi katika uwekezaji wa kibadhirifu na kudhoofisha miundombinu iliyojengwa kwa jasho la umma katika Shirika la Reli (TRL). Nashukuru kwamba wabunge tuliungana pamoja bungeni miaka 50 ya Uhuru kutaka nyongeza ya fedha katika bajeti ya miundombinu; hata hivyo ongezeko hili halitakuwa na tija iwapo hatua stahiki dhidi ya ufisadi katika sekta husika. Katika nyongeza ya bajeti ya miundombinu, pamoja na masuala mengine ya kitaifa nilisisitiza umuhimu wa reli ya kutoka Ubungo mpaka Stesheni kuanza kufanya kazi kwa ajili ya kubeba abiria kama sehemu ya kupunguza msongamano na serikali imekubali kulipa kipaumbele suala hilo.
Mikakati mipana ya kukabiliana na foleni bado inasuasua kwa kuwa katika mwaka wa fedha 2011/2012 fedha kidogo takribani bilioni tano pekee ndizo zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara za pembezeno za kupunguza foleni ambazo zingepunguza kiwango kiwango cha magari katika barabara ya Morogoro. Shughuli pekee ambayo imekamilika baada ya kuipa msukumo ni ujenzi wa daraja la Msewe ambalo limeanza kupunguza foleni kupitia barabara ya Chuo Kikuu.

Katika kipindi cha muda mfupi ni lazima kuweka mkazo zaidi katika ujenzi wa barabara hizo za mzunguko (ring roads) kwa kiwango cha lami na Mfumo wa Usafiri wa Umma (DART). Kabla ya miradi mingine ya muda wa kati kama upanuzi wa barabara ya Morogoro na ujenzi wa njia za mpishano (fly over). Hata hivyo, mikakati yote hii haitawezesha suluhisho endelevu iwapo mipango miji ya Dar es salaam haitazingatia mwelekeo wa muda wa jiji lenyewe na hata taifa kutokana na kasi ya ongezeko la watu hususani kutoka vijijini. Katika kipindi cha mwaka mmoja kama sehemu ya uwakilishi na usimamizi nimehoji kuhusu Mpango Kabambe wa Jiji (Master Plan) na nitaendelea kufuatilia kwa karibu ili tupate msingi wa kuchukua hatua zaidi miaka 50 baada ya uhuru.

Aidha katika kuwezesha hatua za muda mfupi, Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo la Ubungo umeweza kutenga fedha za ukarabati wa baadhi ya barabara za mtaani pamoja na ujenzi wa madaraja ya watembea kwa miguu. Pia, manispaa imeweza kushawishiwa kutenga fedha kwenye bajeti 2011/2012 kuweza kutenga fedha zaidi za ujenzi wa madara katika kata mbalimbali za Jimbo la Ubungo.

Miaka 50 baada ya uhuru hali ya viwanja vyetu vya ndege na shirika la umma la ndege (ATCL) ni ya kuliaibisha. Taifa limeingia katika kugharamia shirika hili kwa maamuzi mabovu katika vipindi tofauti tofauti. Serikali imeshindwa kufanya upanuzi wa Bandari kubwa kwa wakati; badala yake wameingia mikataba mibovu ya upakuzi wa mizigo inayopelekea kupunguza hata kiasi cha shehena kinachohudumiwa katika bandari zetu. Wakati washindani wetu nchi za jirani; wanapanua bandari zao na kuwekeza katika miundombinu, sisi ambao tuko katika nafasi bora zaidi ya bandari zetu kupata soko kubwa la nchi za maziwa makuu tunabaki tumetahayari kutokana na sera legelege na uongozi mbovu.

Wakati wa kudai uhuru, ni vijana makuli wa pale bandarini ndio Dar es salaam waliokuwa mstari wa mbele kwenye kudai uhuru; hawakuigopa serikali dhalimu ya kikoloni kwa kuwa hawakuwa na cha kupoteza kama wenye kazi za kola nyeupe(white collar) waliokuwa kwenye serikali ya mkoloni. Ndio maana huwa nafarijika kila ninapoona vijana wasio na ajira na watanzania wa kawaida kwa ujumla wanapoendelea kuunga mkno mabadiliko ya kweli ili kupata uhuru wa kweli. Tabaka hili, halina cha kupoteza isipokuwa umasikini wao na malipo watakayopata ni kuishi kwenye taifa lenye kutoa fursa.

Miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika tumeendelea kuwa na upungufu wa umeme hali ambayo imeathiri uchumi kwa kupunguza uzalishaji na kuongeza gharama za maisha. Hali hii imetokana na utegemezi wa kiwango kikubwa wa vyanzo vya umeme wa maji vilivyoanzishwa wakati wa serikali ya awamu ya kwanza na kukithiri kwa ufisadi katika ununuzi na mikataba ya umeme wa dharura kwenye awamu zilizofuata za utawala.
Katika kipindi cha mwaka mmoja nimeungana na wengine kuisimamia serikali kuwasilisha bungeni mpango wa dharura wa umeme. Pamoja na mpango husika kuwasilishwa nimeendelea kupinga gharama kubwa kwa mikopo ya kibiashara na utekelezaji wa kusuasua wa mpango wa dharura wa umeme. Hatua hii imeenda sambamba na kushawishi kufikishwa kwa umeme katika baadhi ya maeneo ya jimbo ambayo hayakuwa na umeme kabla.

Badala ya ‘sherehe’ za uhuru zenye kugharimu zaidi ya bilioni 50; nilitarajia kwamba siku hiyo ingetumika kuzindua mitambo mipya ya umeme ya kununua sio ya kukodi ili kuacha alama ya kudumu miaka 50 baada ya uhuru. Kutokana na takribani MW 250 ambazo zilikuwa ziwe zimepatikana kati ya Septemba mpaka Disemba 2011 kutopatikana mpaka hivi sasa nitaendelea kuchukua hatua kuisimamia serikali kutekeleza ahadi ya kuondoa tatizo la mgawo wa umeme.

Aidha, nitaendelea kuwawakilisha wananchi kupinga ongezeko la bei ya umeme la wastani wa asilimia 185 na badala yake kuitaka serikali kuwa na mpango wa kulinusuru Shirika la Umeme (TANESCO) dhidi ya gharama kubwa zinazotokana na mitambo ya kukodi, ufisadi kwenye mikataba , madeni ya serikali na kuhakikisha gharama zinabebwa zaidi na watumiaji wakubwa badala ya watumiaji wadogo wa kipato cha chini.

Miaka 50 baada ya uhuru serikali inajivunia kuboresha miundombinu kwa kutumia takwimu za kuongezeka kwa idadi ya wanaotumia simu za mkononi. Lakini ukitafakari kwa undani ukuaji wa sekta hii utabaini kwamba umetokana na nguvu ya sekta yenyewe kwa sababu za nje ya sera za serikali na hivyo kufanya mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa taifa na hata kubadili kipato cha watanzania mmoja mmoja mwenye simu kuwa ni finyu. Tathmini ya hivi karibuni katika maeneo mbalimbali ya nchi inaonyesha kwamba katika kila watanzania kumi (10) wenye simu, ni watanzania wawili (2) ndio wanatumia simu zao kwa matumizi binafsi na biashara; hivyo asilimia kubwa ya watanzania watumia simu kwa matumizi binafsi pekee na si biashara ama shughuli za uzalishaji.

Miaka 50 baada ya uhuru tunakabiliwa na athari ya kiuchumi ya utegemezi ambao taifa letu limeingizwa kwa kutegemea misaada kutoka nje huku rasilimali za taifa zikifyozwa kibeberu. Hali hii inatuhitaji kwa pamoja tufanye mabadiliko tuwe na uhuru wa kweli.

Mwanafalsafa Frantz Fanon aliwahi kusema kwamba kila kizazi lazima nje ya uvungu uvungu kiutambue utume wake; ama kiutumize au kiusaliti. Kizazi cha wakati huo, kilidai uhuru, na kujenga misingi ya taifa (national building) ingawa misingi hiyo imekuja kuvurugwa na kutuingiza katika ukoloni mambo leo (neo colonialism). Ni wajibu wa kizazi chetu; kudai uhuru wa kweli, uhuru dhidi ya umasikini, ujinga, maradhi; hatuwezi kudai uhuru huo bila kumpiga vita adui ufisadi. Wajibu wa kizazi chetu ni kuweza kupambana katika mazingira ya ushindani wa ndani na nje ya nchi yetu; kujenga taifa tukitazama kizazi chetu na kijacho. Mabadiliko haya tuyafanye katika maeneo mbalimbali ya nchi yenye rasilimali ambayo yameporwa; iwe ni maeneo ya migodi, maeneo ya uwindaji, maeneo ya uwekezaji katika kilimo cha mashamba makubwa.
Miaka 50 baada ya uhuru naiona laana ya rasilimali (resource curse) kuwa ni moja ya visababishi vya kuvunjika kwa amani nchini. Tunaelekea kwenda kuchimba mafuta na madini ya urani; nchi hii iko mashakani kama hatutafanya mabadiliko kimfumo na kiuongozi.

Katika kuchangia mabadiliko kwenye sekta za nishati na madini kwa nafasi ya uwaziri kivuli tarehe 15 Julai 2011 niliwasilisha bajeti mbadala bungeni ambayo baadhi ya mapendekezo yake serikali imeanza kuyafanyia kazi. Hata hivyo, sehemu kubwa ya kasoro bado serikali haijachukua hatua hivyo tunapokwenda tutaongeza nguvu zaidi katika kuhakikisha usimamizi thabiti wa sekta hii ambayo ni mtaji kwa taifa.
Katika kutimiza wajibu wa kibunge wa usimamizi na kutunga sheria zenye kuhakikisha mabadiliko ya kiuchumi nilikuwa mstari wa mbele katika kufanya marekebisho katika Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2011 ili kuweza kuongeza ufanisi na kudhibiti mianya ya ufisadi katika ununuzi wa umma kwenye serikali kuu, taasisi zake na katika serikali za mitaa.

Uhuru na Mabadiliko ya Jamii
Nchi hii imewekwa rehani kijamii; ndoto ya waasisi wa taifa hili la kujenga taifa lenye uhuru na umoja inaanza kufifishwa. Baadhi ya viongozi katika utawala wanatembea kifua mbele wakizusha mijadala ya ukabila na udini yenye kuligawa taifa. Katika hotuba zake mbili za tarehe 9 Disemba 1961 Nyerere alitabiri hali hii kwa kueleza kwamba msingi wa kufanikiwa kwa TANU ulikuwa ni umoja wake na kwamba wanachama wake wakigombana na kutengana mambo yao na mambo ya taifa zima yatakwenda tenge. Umoja kati CCM ya sasa na ndani ya Serikali umetoweka; chama legelege kimezaa serikali legelege.

Miaka 50 ya uhuru chini ya sera mbovu na utawala dhaifu matabaka yanazidi kumea katika taifa, pengo kati ya masikini na matajiri linaongezeka kila kukicha. Uchambuzi unaonyesha kwamba watanzania wameanza kupoteza matumaini ya kuwa na maisha bora; katika kila watanzania kumi, saba wamesema kwamba hali yao ya maisha haijawa bora. Na kati yao; asilimia hamsini hali yao imekuwa mbaya zaidi. Nyufa hizi ni tishio kwa mustakabali mwema wa taifa letu.

Miaka 50 baada ya uhuru, huduma za kijamii zinazidi kudorora; kwa kiwango cha huduma hizo na hata upatikanaji hususani kwa watanzania masikini. Elimu ni sehemu ya uhuru wa kweli kwa vijana; kwa Tanzania ya leo mfumo mzima wa elimu ujenga matabaka. Katika kipindi cha mwaka mmoja wa utumishi wa umma nimetembelea shule za kata mbalimbali za jimbo la Ubungo na kubaini matabaka kuanzia chekechea mpaka sekondari; baina ya shule binafsi na za umma, utofauti wa mazingira ya kusomea na maslahi ya walimu ni kubwa.

Nilichobaini ni kwamba ruzuku ya bajeti ya elimu kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari (capitation grant) kwa kiwango cha kutosha na hata inayofika haifiki kwa wakati na pia hakuna uthibiti makini wa matumizi. Hili ni eneo ambalo nitalipa uzito wa pekee tuendako. Pamoja na kuongezeka kwa idadi ya madarasa katika shule za umma, bado kuna tatizo la ubora wa madarasa yenyewe yaliyojengwa kwa ukilinganisha na kiwango cha fedha za michango ya wananchi zilizotumika. Kwa kushirikiana na madiwani tumesimamia na kubaini ujenzi wa madarasa hewa na pia kiwango duni cha majengo ya kipindi kilichopita ikiwemo vyoo katika mashule na hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ikiwemo baadhi ya wakandarasi kulazimishwa kukamilisha kazi husika.
Pia, baada ya kubaini hali hiyo tumejadiliana na madiwani kuweza kuwa na kampeni maalum ya kumaliza tatizo la madawati katika shule za msingi na sekondari katika jimbo na manispaa kwa ujumla. Kwa kushirikiana na meya maamuzi yalifanyika ya kuchukua fedha kutoka mafungu mengine ya halmashauri kwa ajili ya kutengeneza madawati kwa wingi na kusambaza katika shule mbalimbali. Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo la Ubungo nao umetoa sehemu ya madawati. Madawati hayo yameanza kusambazwa kwa awamu katika shule mbalimbali. Orodha ya madawati kwa shule zilizopatiwa itatolewa katika taarifa ya utendaji kwa kila kata.

Kwa upande wa elimu ya juu; vijana wa vyuo vikuu ni wajibu wao kuwa mstari mbele kuendelea kuunga mkono mabadiliko, kwani ni mashuhuda wa namna ambavyo serikali inavyofanya matumizi ya anasa, fedha za umma zikipotea kwa ufisadi. Hatima ya yote mzigo unarudi kwa mwanafunzi na wazazi wake kupitia sera za uchangiaji ambao wengine imewanyima fursa ya kusoma. Katika kipindi cha mwaka mmoja, nimefanya kazi ya kuwakilisha masuala mbalimbali ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa ajili ya kupata majibu ya serikali bungeni. Hata hivyo, majibu hayo pamoja na kuweza kutatua baadhi ya matatizo hayo hayajaweza kutoa suluhisho la kudumu hali ambayo imefanya migomo ya kudai haki miongoni mwa wanachuo ikiwemo wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuendelea.
Pia, kuna udhaifu mkubwa katika mfumo wa bodi ya mikopo kwa kiwango ambacho wapo wanafunzi ambao katika mazingira ya kawaida wangepewa kipaumbele katika mikopo lakini hawajapata mikopo. Hivyo, tofauti na ahadi ya Rais kwamba hakuna mtoto wa maskini atayeshindwa kusoma kutokana na kukosa mikopo wapo watoto wa maskini ambao wameshindwa kuendelea na masoko. Tumeweza kuchangia baadhi yao kupitia Mfuko wa Elimu Ubungo unaochangiwa asilimia 20% ya mshahara wa mbunge kwa mwezi lakini maombi na mahitaji ni mengi zaidi.

Hali hii iko hivi wakati ambapo toka Januari mpaka Disemba 2011 kwa ajili ya ‘sherehe’ za uhuru serikali ikiwa imetumia fedha ambazo zingeweza kulipia mikopo wanachuo zaidi ya elfu hamsini na kubaki. Fedha hizi zimetumiwa kuanzia kwenye maonyesho ya Wizara na Taasisi zake huku matumizi yakijirudia rudia wakati wa maonyesho ya kila Wizara pekee, wakati wa Saba Saba na wakati wa maonyesho maalumu ya mwezi Desemba.

Tunapokwenda nitaendelea kuwakilisha na kuwasilisha masuala ya wanafunzi wa elimu ya juu ikiwemo kutaka ripoti ya tume ya Rais kuhusu mikopo iwekwe wazi hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kuboresha mfumo wa ugharamiaji wa elimu ya juu. Aidha, mwaka 2012 nitaunganisha nguvu ya wadau wengine ili kupanua wigo na ufanisi wa mfuko wa elimu Ubungo ili kuwa na uwezo wa kunufaisha wanafunzi wengi zaidi wa msingi, sekondari, vyuo pamoja na elimu ya mtaani kwa vijana na wanawake.

Kwa kipindi cha miaka 50 katika Jiji la Dar es salaam uwezo wa kupata maji kutoka makampuni na taasisi za umma ambazo zimekuwa zikibadilika majina katika nyakati mbalimbali toka uhuru unapungua badala kuongezeka. Maelezo yanayotolewa ni kwamba kuna upotevu wa maji kutokana na mitambo michakavu kwa kuwa imejengwa mara baada ya uhuru na kwamba kasi ya ongezeko la watu hailingani na kiwango cha upanuzi wa miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa maji. Ikiwa hali hii ipo katika jiji la Dar es salaam itachukua miaka mingapi ya uhuru kuweza kuhakikisha kila mtanzania anapata maji safi na salama na pia miundombinu ya maji taka inakuwepo katika miji yetu.

Ili kuchangia kupata ufumbuzi mwezi Januari 2011 niliwaita pamoja wadau katika Kongamano la Maji Jimbo la Ubungo na maazimio ya kongamanao hilo ulikuwa msingi wa ufuatiliaji jimboni, bungeni na kwenye mamlaka mbalimbali kwa kipindi cha mwaka mmoja. Baada ya kuona utendaji kazi wa mamlaka husika una sua sua ilinibidi kama sehemu ya uwakilishi na usimamizi niunganishe nguvu ya umma kuweza kwenda Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASCO) kuweza kupata majibu ya msingi ya hatua ambazo zimechukuliwa. Matokeo ya jitihada zote ni kufanyika kwa operesheni maalum ya kushughulikia biashara haramu ya maji pamoja na kuongeza mgawo wa maji ambayo imesaidia baadhi ya maeneo ambayo awali yalikuwa hayapati maji na sasa yanapata kwa vipindi.

Hata hivyo, yapo maeneo ambayo mpaka sasa hayajaweza kupata maji hivyo jitihada zaidi zinahitajika katika mwaka 2012; ikiwemo kukabiliana na ufisadi katika sekta ya maji, Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) kuongeza kasi katika uwekezaji kwenye uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa maji na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuweza kudhibiti bei za maji. Katika kipindi husika tumefanya vile vile ufuatiliaji na kubaini udhaifu mkubwa zaidi katika usimamizi wa miradi ya maji ya jumuia hali ambayo imefanya wananchi kukosa maji; kama sehemu ya uwakilishi nimezisimamia mamlaka husika katika Manispaa kuchunguza miradi hiyo na hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa katika kata husika. Kwa upande mwingine miradi ya washirika wengine kwenye kata ambayo ilikwama kwa miaka mingi ya uchimbaji wa visima virefu na usambazaji wa mabomba ya maji imesimamiwa na iko kwenye hatua za mwisho za kuanza kufanya kazi katika kata mbalimbali.

Miaka 50 ya uhuru wananchi wanapoteza kwa wingi maisha yao kwa wingi kwa magonjwa yanayoweza kutibika kama malaria. Pamoja na sera ya uchangiaji kuwa mzigo wa watanzania walio wengi bado vifaa na madawa havipatikani hususani katika hospitali na zahanati za umma.

Familia za maskini ambazo zimepoteza wanawake wajawazito au watoto wakati wa kujifungua kutokana ubovu wa huduma za afya wanaweza kuelezea vizuri zaidi hali ya sekta ya afya nchini. Jitihada za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo la Ubungo kujenga kituo cha Afya ya Mama na mtoto Jimboni ni sehemu tu ya mfano kwa serikali kuchukua hatua zaidi kuweka mazingira bora zaidi kwa wakina mama na watoto katika zahanati na vituo vya afya kwa kila kata.

Aidha, baadhi ya athari za kiafya zimekuwa zikichangiwa na matatizo katika uchafuzi wa mazingira. Kwa upande mmoja kumekuwa na uchafuzi wa mazingira kutokana na udhaifu katika mfumo mzima wa maji taka katika jiji la Dar es salaam lakini kwa upande mwingine kutokana na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na viwanda. Katika kipindi cha mwaka mmoja, niliweka mkazo katika uchafuzi wa mazingira unaotokana na utiririshaji wa maji taka toka kwenye Hosteli za Chuo Kikuu eneo la Mabibo kwenda kwenye Mto Kisiwani pamoja na uchafu katika mabwawa ya maji taka eneo la Mabibo. Nimetembelea maeneo husika na nimezisukuma mamlaka husika kuchukua hatua kwa nyakati na njia mbalimbali. Hatua hizo zimeweza kupunguza ukubwa wa matatizo kwa muda, hata hivyo katika mwaka 2012 nitaendelea kuzifuatilia mamlaka husika ili kuweza kuwa na suluhisho la kudumu.

Kwa upande mwingine, matatizo ya afya mazingira yameendelea kushamiri kutokana na kukithiri kwa uchafu katika jiji la Dar es salaam. Matatizo hayo yanachangiwa na udhaifu katika mfumo mzima wa uzoaji, ukusanyaji, usafirishaji, uhifadhi na utumiaji wa takataka. Mfumo mpya wa Manispaa kujitoa katika uzoaji wa moja kwa moja wa taka katika maeneo mengi na badala yake kubaki na jukumu la uratibu bila kufanya maandalizi ya kutosha kwa serikali za mitaa na wananchi wa maeneo husika umesababisha migogoro na uchafu katika maeneo mengi. Kutokana na hali hii, nilitoa pendekezo la tathmini kuweza kufanyika kwa mfumo mzima na hatua mbadala kuchukuliwa. Kufuatia pendekezo hilo manispaa ya Kinondoni tayari imekutana na wenyeviti na watendaji wa mitaa kufanya tathmini husika; hata hivyo, bado hatua za ziada zinahitajika katika mwaka 2012 kuweza kupunguza matatizo ya uchafu hatua ambazo zinapaswa pia kuhusisha kuongeza vifaa na kuboresha mfumo mzima ikiwemo wa ushirikishwaji wa wananchi. Kwa upande mwingine, kuna matatizo ya gharama kubwa ya uzoaji taka kutokana na umbali wa usafirishaji wa taka na pia changamoto katika madampo mbalimbali. Ili kupunguza matatizo haya, ni muhimu katika mwaka 2012 kuongeza kasi ya kuwa na dampo mbadala kwa ajili ya Manispaa ya Kinondoni ili liweze pia kuhudumia kata mbalimbali za jimbo la Ubungo kwa ukaribu zaidi.

Kwa ujumla huduma za kijamii iwe ni elimu, afya au maji zimegeuzwa kuwa bidhaa za ghali na adimu. Ni muhimu kuwa na mfumo wa uchumi wa jamii ya kwamba hata katika soko ni lazima kwa taifa kuwa na mifumo ya ulinzi wa kijamii (social security) inayogusa makundi mbalimbali katika maeneo mbalimbali ya huduma za kijamii.

Miaka 50 baada ya uhuru ahadi za kutoa fursa pana kwa makundi maalum mathalani wanawake, wazee, vijana na wenye ulemavu kuweza kujiendeleza zimekuwa ni maneno matupu bila vitendo. Sera zinazotekelezwa zinayatazama makundi haya kama watu tunaohitaji kusaidiwa badala ya kuwa wadau wa msingi wa kimaendeleo.

Kwa kutambua hali hii katika michango yangu bungeni niliweka mkazo wa pekee katika masuala ya wanawake ikiwemo yanayohusu Benki ya Wanawake na kutaka pia pawepo na Benki ya Vijana wazo ambalo serikali imelikubali. Hata hivyo, uwepo wa benki hizi unapaswa uongezewe nguvu kwa mabadiliko ya kimfumo na kiutaratibu katika taasisi mbalimbali za fedha kuweza kupanua wigo kwa makundi haya ya kijamii kujikwamua kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wangu, katika kipindi cha mwaka mmoja nimeendelea kushirikiana na wanawake na vijana katika kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo jimboni. Kutokana na hali hii pamoja na michango toka fedha binafsi za mbunge kwa ajili ya vikundi mbalimbali vya vijana na wanawake nimeweza kutenga fedha toka kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kwa ajili ya Muungano wa VICOBA 100 vya Jimbo la Ubungo kwa ajili ya kukopeshana. Aidha, nimedhamini mashindano mbalimbali ya michezo kwa wanawake na kwa vijana katika maadhimisho mbalimbali jimboni Ubungo. Hatua hizi zote hazijitoshelezi ukilinganisha na idadi ya wanawake na vijana jimboni pamoja na ukubwa wa matatizo ya ukosefu wa ajira na fursa za kujiendeleza miongoni mwa wanawake na vijana jimboni hivyo katika mwaka 2012 nitaweka mkazo maalumu kwa ajili ya mabadiliko ya kimfumo lakini pia katika kuunganisha nguvu za wadau wengine zaidi ili kuchangia katika maendeleo.

Tunapokwenda tuweke pia mipango ya kuhakikisha badala ya wazee wetu kuonekana kuwa kundi linalopaswa tu kubebwa na kuhudumiwa, sera mbadala zitaboresha kiwango na mifumo ya malipo ya wastaafu na kupanua wigo wa mifuko ya kijamii kujumuisha ajira ambazo haziko kwenye mkondo rasmi ikiwemo kilimo ili kutoa pensheni kwa wazee wote. Katika kipindi cha mwaka mmoja nimeshiriki kuwakilisha hitaji la uboreshaji wa mifumo ya wastaafu ili kuwezesha wazee wetu kuwa na fursa ya kupata huduma za msingi na kuwa na kipato stahili cha kuwakimu hata baada ya kumaliza utumishi wao kwa taifa
Miaka 50 ya Uhuru, vyombo vya ulinzi na usalama vimeweza kulinda mipaka ya nchi yetu ilipovamiwa na Iddi Amin wa Uganda katika vita ya Kagera. Hata hivyo, nafasi ya vyombo vyetu katika kulinda maslahi ya nchi na kudhibiti masuala yenye kulihujumu taifa inaanza kuporomoka. Ni muhimu kwa vyombo vya ulinzi na usalama kujitafakari na kuweka mstari wa mbele kulinda maslahi ya umma badala ya matakwa ya mafisadi. Vyombo vya dola ambavyo vinapaswa kutimiza wajibu huu kwa ukaribu zaidi ni Usalama wa Taifa (TISS), TAKUKURU na Jeshi la Polisi kwa kuweka mkazo masuala ya kiuchumi na kijamii katika kazi zao ndani na nje ya mipaka yetu.

Katika kipindi cha mwaka mmoja wa utumishi wa umma, nimekuwa nikivikumbusha vyombo husika bungeni na kwa njia nyingine mbalimbali za uwakilishi kuweza kuchukua hatua stahiki kuhusu masuala mbalimbali. Aidha, nimechangia jitihada za kuimarisha ulinzi jimboni dhidi ya vitendo vya ujambazi na uhalifu wa aina nyingine kwa kushiriki katika harambee za ujenzi wa vituo vya polisi pamoja na ulinzi shirikishi. Pia, nimeweka mkazo katika kuunga mkono jitihada za kuboresha maslahi ya askari ikiwemo kushughulikia malalamiko ya madai ya malipo pungufu ya posho na malimbikizo ya madeni mbalimbali. Tuendako ni muhimu pia kuweka mkazo katika ujenzi wa kituo cha kisasa cha polisi cha ngazi ya wilaya jimboni Ubungo.

Miaka 50 baada ya uhuru pigo lingine kwa mwelekeo wa taifa letu, na utumwa wa kiutamaduni unaoendelea kumea. Vijana wanaweza kubebeshwa mzigo wa lawama wa kuiga tamaduni za kigeni kwa kiwango chenye kupoteza utaifa wetu; ukweli ni kuwa chanzo cha yote haya ni uongozi usio na maono. Unapokuwa na utawala wenye sera ambazo hata vyombo vya habari vya umma vinakuwa kinara wa kuwa vioo vya tamaduni za nchi zingine; usitegemee vijana kubeba urithi wa nchi yao.

Tuendako viongozi wetu wanapaswa kuelewa kwamba nchi zilizofanya mapinduzi ya kiuchumi; muhimili thabiti wa mwelekeo wao ni tamaduni zao. Kinyume chake, nchi zenye viongozi wabinafsi; viongozi wasiojiamini, viongozi wasiowajibika ambayo ni matokeo ya utamaduni wa ufisadi.

Ni muhimu tukaungana kuendelea kufanya mabadiliko ili kuweka mkazo katika kujikwamua kifikra; kuanzia katika desturi zetu; fasihi zetu; muziki wetu; michezo yetu; familia zetu: vyote vituelekeze katika kujenga taifa lenye kukumbuka tulipotoka na kutengeneza mweleko mwafaka wa vizazi vijavyo.

Uhuru na Mabadiliko ya Siasa:
Tarehe 9 Disemba 1961 bendera ya wananchi wa Tanganyika yenye rangi tatu za kijani kibichi, nyeusi na dhahabu kama ishara ya uhuru wa kisiasa wa kujitawala.
Baada ya Uhuru, viongozi wa kwanza wakiongozwa na Mwalimu Nyerere walianza mikakati ya kujenga taifa (National Building) kwa kuchukua maamuzi muhimu ya kuleta umoja. Maamuzi hayo yaliongozwa na dhana kama ‘uhuru na umoja’, ‘uhuru na kazi’ na hata baadaye ‘uhuru na maendeleo’; huku kauli mbiu kama ‘siasa ni kilimo’ zikitumika kusukuma ajenda husika.

Baadhi ya maamuzi makubwa ya kisiasa ni pamoja na: Muungano katika ya Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964; kufutwa kwa Mfumo wa Vyama vingi mwaka 1965; kutangazwa kwa Azimio la Arusha mwaka 1967 kulikofuatiwa na utaifishaji (nationalization) wa njia kuu za kiuchumi- kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kufuata siasa ya ujamaa na kujitegemea; kufutwa kwa dhana ya serikali za mitaa mwaka 1972 na kuanzishwa kwa madaraka mikoani nk. Kwa ujumla kati ya kipindi cha mwaka 1961 mpaka 1985 taifa lilioongozwa kufanya maamuzi mengi ya kisiasa yenye taathira kubwa ya kiuchumi na kijamii ambayo inaonekana hadi leo. Si lengo la waraka huu kuchambua kila uamuzi na faida na hasara zake; katika kipindi husika ambacho Urais wa taifa letu uliongozwa na Mwalimu Julius Nyerere.

Miaka 50 baada ya uhuru kwa ujumla maamuzi mengi yaliyofanyika wakati huo yaliwezesha kujengwa kwa taifa lenye umoja, amani na mshikamano; hata hivyo maamuzi hayo hayo yamedumaza utamaduni wa ushindani katika taifa letu iwe ni kwenye sekta za kiuchumi na hata siasa yenyewe. Mathalani, uamuzi wa kufanya chama kishike hatamu, ulifanya moja kwa moja taasisi ambazo zinapawa kuwa huru kugeuzwa kuwa mihimili ya chama kinachotawala; kuanzia vyama vya wafanyakazi, asasi za kiraia na hata jeshi ambalo baada ya maasi (mutiny) ya mwaka 1964, jeshi mpya la wazalendo (JWTZ) liliundwa na askari kutoka umoja wa vijana wa TANU (TYL). Uhuru wa fikra uliminywa kiitikadi, kisheria na kimatendo kwa kutumia kivuli cha kutaka kujenga umoja wa kitaifa. Wakati huo huo, katika kipindi husika kuliendelezwa kwa kiasi kikubwa sheria na mfumo wa utawala tuliorithi kutoka kwa mkoloni.

Awamu ya Pili ya Utawala Tanzania kati ya mwaka 1985 mpaka mwaka 1995 chini ya Rais wa wakati huo- Ali Hassan Mwinyi; nao ulikuwa na maamuzi yake ambayo ni muhimu kukumbukwa kihistoria.

Kwa kiasi kikubwa maamuzi hayo ya kisiasa yakifanyika kwa shinikizo kutoka nje, ambapo maamuzi ya kiuchumi ndiyo kwa kiwango kikubwa yaliyokuwa yakiamua hatma ya mwelekeo wa kisiasa. Kwa masharti ya Benki ya Dunia (WB) na Taasisi ya Fedha ya Kimataifa (IMF), Tanzania ikafanya ‘geuka nyuma’ ya kisiasa, kwa maelezo ya kufuata sera za ubinafsishaji na soko huria. Lakini mageuzi hayo yalikuwa ni barakoa (mask) ya kutupeleka kwenye utamaduni wa ubinafsi na soko holela.

Kati ya matukio ya kukumbukwa wakati huo ni pamoja na: Maamuzi ya Zanzibar ya mwaka 1991 ambayo yalifuta misingi muhimu ya Azimio la Arusha, hususani iliyohusu maadili ya uongozi na nchi kuingia katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Hata hivyo, mageuzi yote hayakuendena na kuandikwa kwa katiba mpya, na matokeo yake ni sheria na hata utamaduni wa kisiasa kuendeleza misingi ya chama tawala kuwa chama dola; mithili ya nchi kuendelea kuwa katika mfumo wa chama kimoja. Ripoti za Tume ya Nyalali na Tume ya Kisanga zinaweza kutupa picha ya ziada ya hali ya kisiasa katika kipindi husika na maamuzi ambayo yalipaswa kufanyika miaka 50 baada ya uhuru.

Awamu ya tatu ya utawala chini ya urais wa Benjamin Mkapa kati ya mwaka 1995 mpaka mwaka 2005 ulitaasisisha misingi ya soko holela na ubinafsi na hivyo kuliondoa taifa katika misingi ya uwajibikaji na kulitumbikiza katika utamaduni wa ufisadi. Ukiweka katika mizani, mafanikio ya Mkapa katika kuweka misingi ya kiuchumi iliyojikita zaidi katika utandawazi, uwekezaji wa kigeni na unyonyaji wa kodi toka kwa wananchi masikini hayawezi kulingana na hasara ya ufisadi na uuzaji wa rasilimali ambao ulifanyika katika awamu yake ya utawala. Ni katika kipindi hicho hicho ambacho maamuzi ya siasa zetu katika uchaguzi, yameanza kuwekwa katika nguvu zilizo nje ya nguvu ya umma wa watanzania miaka 50 baada ya uhuru wa Tanganyika.

Awamu ya nne imeingia mwaka 2005 chini ya Rais Jakaya Kikwete na kuahidi kuendeleza yale yaliyoachwa na awamu ya tatu kwa ari, nguvu na kasi mpya; na mwaka 2010 kuendeleza zaidi pale ambapo utawala wake umefikia. Tarehe 9 Disemba 1961, Nyerere aliiasa TANU dhidi ya kupoteza wakati katika kugombania vyeo na fahari ya nafsi; hali ambayo sasa imeikumba CCM na kuathiri mwelekeo wa chama tawala katika kuisimamia serikali iliyo madarakani.

Miaka 50 baada ya uhuru wa Tanganyika nchi yetu inakabiliwa na changamoto nyingi za kisiasa na kiutawala zenye taathira kubwa katika maendeleo ya taifa letu na watu wake.

Bado taasisi muhimu katika nchi yetu hazijaweza kutoa uongozi wa kisiasa na hivyo kufanya taifa kudumbukia katika siasa chafu na utawala mbovu katika ngazi mbalimbali. Ombwe hili la uongozi, lenye ishara zote za kushindwa kufanya maamuzi bora katika masuala ya msingi yanayolikabili taifa; limesababisha misingi ya haki na utawala wa sheria inazidi kutetereka.

Toka orodha ya mafisadi (list of shame) isomwe mnamo Septemba 15, 2007; mafisadi wameendelea kuachwa wakitamba na kuliteteresha taifa. Mtiririko wa matukio unaonyesha kwamba vikao vya juu vya chama kinachotawala vimetekwa mafisadi hali ambayo inaelekea kujipenyeza mpaka kwenye mihimili mingine ya dola. Kuachwa kwa hali hii miaka 50 baada ya uhuru kumefanya mazoea ya ufisadi kusambaa kwenye ngazi mbalimbali za serikali na taasisi nyingine badala ya taifa kuwa na utamaduni wa uwajibikaji.

Katika kipindi cha mwaka mmoja ya utumishi wa umma nimehoji kwa njia mbalimbali hatua za serikali kuhusu ufisadi kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kupitia kampuni ya Kagoda, Kampuni ya Meremeta, uuzwaji kinyemela wa Shirika la Usafiri Dar es salaam (UDA), mikataba mibovu kwenye kituo cha Mabasi cha Ubungo (UBT), Richmond/Dowans, upotevu wa mapato katka gesi asilia hususani kuhusu kampuni ya Pan African Energy, malipo kwa Twiga Chemicals nk. Tunapokwenda nitaendelea kushirikiana na wote wenye kupinga ufisadi ili kuhakikisha hatua za msingi zinachukuliwa kwa ajili ya kuwezesha wimbi la uwajibikaji katika ngazi mbalimbali za utumishi wa umma.
Miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika katika kutafuta uhuru wa kweli wa kisiasa tuendelee kusimamia mabadiliko ya katiba ili tuweze kubadili sheria na mazingira ya kisiasa. Hii ihusishe mabadiliko ya mfumo wa kiutawala kuondokana na misingi iliyorithiwa kwa mkoloni wa kuwapa madaraka makubwa viongozi wa kuteuliwa kama wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa; hodhi ya utawala ikiwa kwa serikali kuu badala ya kuongozwa kwa nguvu ya umma kupitia viongozi waliochaguliwa na umma kidemokrasia.

Katika kipindi cha mwaka mmoja nimeshiriki katika kusukuma suala la mabadiliko ya kimfumo kwa kutaka kuanzishwa kwa mchakato wa katiba mpya wenye kuwahusisha wananchi. Wakati serikali ilipotaka kuanza mchakato moja kwa moja kwa mamlaka ya Rais bila kuwa na sheria wala kuhusisha vyombo vingine vya uwakilishi nilipinga kwa nguvu suala hili na kueleza kusudio la kuwasilisha hoja binafsi bungeni. Hatua hii ilifungua mjadala mpana na hatimaye serikali ikakubali suala husika kuanzia bungeni kwa kutungiwa sheria. Pamoja na kasoro zote zilizojitokeza baadae muswada wa sheria husika kupelekwa bungeni ni suala ambalo limesaidia katika kupanua wigo wa mjadala, kuwezesha utaratibu kuwekewa mfumo wa kisheria na pia kufanya dhamira ya serikali kutaka kuhodhi mchakato kuonekana bayana kwa watanzania.

Tarehe 5 Novemba 2011 kabla ya kwenda kwenye mkutano wa tano wa Bunge uliojadili Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba nilifanya Mkutano wa Wananchi jimboni kuweza kupata maoni kuhusu muswada huo. Mkutano huo ulivamiwa na polisi ambao walikamata viongozi waandaji, wakakata nyaya za vipaza sauti na kuondoka pamoja na gari la matangazo pamoja na nyaraka za katiba.

Licha ya hali hiyo nilipofika kwenye eneo la mkutano niliendelea kuhutubia wananchi bila kipaza sauti na kupata maoni yao ambao kwa ujumla wao walipinga muswada huo na kunitaka nisusie kwenda kuujadili mpaka pale umma utakapopata muda wa kutoa maoni ya kuuboresha. Ni msimamo huo ndio niliokwenda nao bungeni ambapo muswada ulipitishwa bila kuwa na mjadala wenye tija na Rais akasaini sheria husika hata baada ya kupokea ushauri wa kamati ambayo mimi nilishiriki.

Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 ina vifungu vyenye kukinzana na haki za msingi za binadamu kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa na katiba ya nchi yetu na haijengi muafaka wa kitaifa wa kupata katiba mpya. Pia, muundo na uwakilishi katika Tume na Bunge Maalum ya katiba ulivyo katika sheria husika hautawezesha maandalizi ya rasimu na hatimaye utungaji wa katiba bora ya nchi yetu. Hatimaye kura ya maoni ya kuhalalisha katiba husika itasimamiwa na tume ya sasa ya uchaguzi bila kuwa na muundo na mfumo huru na wa haki wa kitaasisi na kisheria wa kura husika.

Ni muhimu kwa maslahi ya umma tuungane pamoja kutaka kwanza mabadiliko ya msingi ya sheria husika kwa kuwashirikisha wananchi kabla ya mchakato wa katiba kuanza ili taifa lisiingie katika hasara ya kugharamia mchakato ambao utaleta katiba mbovu na migogoro katika nchi.

Uhuru na Mabadiliko:
Ili uhuru wetu uweze kuwa wenye matokeo kwenye maisha yetu na ya taifa letu tunahitaji kuungana kufanya mabadiliko ya kweli. Changamoto kubwa ambayo nimeiona ni kwamba kuna udhaifu katika mifumo yetu ya kiserikali kwenye ngazi mbalimbali hali ambayo inakwaza hatua za haraka za kuleta mabadiliko.

Kwa pamoja tunapaswa kuendelea kulitoa taifa letu katika kufilisika kimaadili na kiitikadi na kukubaliana tunu za kitaifa zenye kuwezesha misingi ya uwajibikaji. Uhuru wa kweli wa kisiasa utakuja kwa kuwa na uongozi wenye maono (vision) na maadili (values) na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika kipindi cha kuanzia sasa na kuendelea kutuwezesha kunufaika na rasilimali zetu: iwe ni vipaji vyetu, kodi zetu au maliasili za nchi yetu.

Binafsi, jambo kubwa ambalo nimelifanya katika kipindi cha mwaka mmoja ni kutimiza majukumu ya kibunge ya uwakilishi, usimamizi na kutunga sheria kwa kuwa na utaratibu wa kufanya mikutano na wananchi, kuwa na ofisi ya mbunge inayohudumia umma na kuwasilisha masuala husika kwa kwa mamlaka mbalimbali bungeni, maofisini, manispaa na kwa njia nyingine mbalimbali. Ni dhamira yangu kuendeleza uwajibikaji tunapokwenda ili kuunganisha nguvu ya umma kila mmoja aweze kutimiza wajibu kwa nafasi yake.

Nihitimishe kwa maneno ya Nyerere kwa taifa siku ya uhuru wa Tanganyika tarehe 9 Disemba 1961 akiwaeleza wananchi kuhusu utendaji kazi wa baraza lake dogo la mawaziri 11 tu: “..mimi na wenzangu ni watumishi wenu ninyi mnaonisikiliza. Tunajua kuwa mnatuamini, nanyi tunawaamini. Na ni ninyi mnaotupa nguvu zetu tunazozihitaji kwa kazi kubwa iliyo mbele yetu…Na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu tutajitahidi kuwatumikieni bila kujitafutia faida zetu wenyewe au fahari ya cheo”. Uhuru na Kazi, Uhuru na Mabadiliko.

Nawatakia heri ya mwaka mpya wenye upendo, furaha na mafanikio tukiweka mstari wa mbele ukweli, uadilifu, na uwajibikaji katika maisha yetu.
Wenu katika utumishi wa umma,
John MNYIKA (Mb)
26/12/2011
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. PICHA NA HABARI - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger